Serikali itaendelea kutoa fedha za kuboresha miundombinu ya Vyuo vya Ufundi ili wanafunzi wa Kitanzania waendelee kupata elimu katika mazingira bora. Hayo yamesemwa Jijini Arusha na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la maabara, madarasa na ofisi (Ufundi Tower) katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC). Amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha sekta ya Elimu kuanzia Awali hadi Vyuo Vikuu kwa wanafunzi wa kawaida na wenye mahitaji maalum.
"Tumejenga madarasa, mabweni, maabara za masomo ya sayansi, tumeongeza nyumba za walimu, majiko na mabwalo ili watoto wa Kitanzania waweze kupata elimu bora bila changamoto yoyote," amesema mhe. Majaliwa.
Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa Serikali pia inafanyia kazi suala la upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya Diploma kupitia tume ya kutathmini iliyoundwa na Wizara ya Elimu ili kuona namna ya kuweza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ngazi ya kati.